Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran yako karibu kufikiwa.
Hayo yamesemwa na Rais Donald Trump ambaye awali alitishia kuishambulia Iran kwa nguvu kubwa zaidi.
Akiwahutubia wanahabari jijini Washington jana Alhamisi, Trump aliashiria kuwa sasa amefuta mashambulizi hayo akiongeza kuwa viongozi wa ngazi ya juu wa Iran wameridhia masharti ya makubaliano hayo.
Aliongeza kuwa ana imani kiongozi mkuu wa Iran ameidhinisha makubaliano hayo yanayoweza kutiwa saini barani Ulaya.
Awali, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani, CENTCOM ilianzisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa kusudi la kujibu shambulizi la awali ambapo helikopta ya jeshi la Marekani iliangushwa.
Kwenye ujumbe katika mitandao ya kijamii Jumanne wiki hii, CENTCOM ilisema hatua hiyo ni “mwitikio mwafaka wa uchokozi usio halali wa Iran.”
Afisa mmoja wa Marekani alinukuliwa akisema mashambulizi hayo yalilenga mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran na rada iliyo karibu na Mlango Bahari wa Hormuz.
Akizungumzia mashambulizi hayo, Trump alisema Iran ilidungua helikopta ya Apache wakati ikishika doria karibu na mlango bahari huo.
Ni hali iliyoweka kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran kwenye njia panda.
Upande wa Iran ulinukuliwa ukisema nchi hiyo bado haijafikia hitimisho juu ya makubaliano na Marekani.