Balozi Dkt. Monica Juma kutoka Kenya amekula kiapo cha kuhudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Vienna, UNOV na Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa juu ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu, UNODC.
Hadi kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo, Dkt. Juma alihudumu kama mshauri wa Rais William Ruto wa masuala ya usalama.
Dkt. Jumaalikula kiapo cha utendaji kazi mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN António Guterres katika hafla iliyofanyika katika makao makuu ya umoja huo jijini New York nchini Marekani.
Akizungumza wakati hafla hiyo, Dkt. Juma aliahidi kutumikia wadhifa wake mpya kwa uadilifu, usawa na kwa kuzingatia madhumuni na kanuni za UN.
“Nachukua wadhifa huo kwa unyenyekevu, shukrani na hisia kubwa ya uwajibikaji, na ninatazamia kufanya kazi na wafanyakazi wenzangu na washirika katika mfumo wa UN, na dunia kuendeleza amani, usalama, haki na utawala wa sheria kwa ajili ya mustakabali wenye ustawi na uadilifu zaidi kwa wote,” aliahidi Dkt. Juma.
Dkt. Juma ni mwanadiplomasia mbobezi kutoka Kenya ambaye pia aliwahi kuhudumu katika nyadhifa za ngazi za juu serikalini ikiwa ni pamoja na kuhudumu kama Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Mambo ya Nje.
Pia aliwahi kuhudumu kama Balozi wa Kenya katika nchi za Ethiopia na Djibouti na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika, (AU), IGAD, na Tume ya Kiuchumi ya UN barani Afrika kati ya mwaka 2010 na 2013.