Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Johana Kiplangat Tonui, ameteuliwa kuwa kamanda mpya kikosi cha General Service Unit (GSU), kwenye mabadiliko ambayo yametekelezwa na Huduma ya Taifa ya Polisi.
Tonui, ambaye awali alikuwa Mkurugenzi wa Operesheni, anachukua wadhifa huo kutoka kwa Ranson Lolmodooni, katika mabadiliko hayo ambayo yamewaathiri maafisa watatu wakuu wa polisi.
Kwenye mabadiliko hayo, Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja, pia amemteua Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Fredrick Egesa Nyongesa, kuwa Naibu Kamanda wa kikosi cha GSU.
Wakati huo huo, Paul Maingo Mumo ameteuliwa kuongoza kitengo cha kushughulikia maswala ya ndani (IAU).
Katika arifa hiyo iliyotolewa Juni 10,2026, Kanja alisema Bodi ya Huduma ya Taifa ya Polisi imeidhinisha mabadiliko hayo na yanatekelezwa mara moja.
Hayo yanajiri baada ya mabadiliko kufanywa kwenye kikosi cha maafisa wa kumlinda rais, wiki chache zilizopita.