Wabunge katika Bunge la Taifa wamempongeza Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kutokana na juhudi zake zilizofeli za kugombea wadhifa wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Wakiongozwa na Spika Moses Wetang’ula, wabunge hao walimsifu Raila kutokana na ujasiri wa kugombea wadhifa huo na kupigania maadili ya bara la Afrika.
Aidha, wabunge wamempongeza Mahamoud Ali Youssouf kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa AUC.
“Bunge hili linampongeza Mheshimiwa Mahamoud Ali Youssouf kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti wa AUC Jumamosi, Februari 2025,” alisema Wetang’ula.
Kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah akitumia fursa hiyo kupuuzilia mbali madai ya utoaji rushwa na kwamba hatua ya kumuidhinisha Raila kugombea wadhifa huo ilichochewa kisiasa.
“Rais Ruto hakuamua kumuunga mkono Raila Odinga kwa sababu alikuwa mshindani wake katika uchaguzi uliopita au kwa sababu wote walikuwa katika chama cha ODM. Aliamua kumuunga mkono Raila kama Mkenya aliyestahiki wadhifa huo na kama mwanasiasa mweledi kutoka Afrika,” alisema Ichung’wah.
Kwa upande wake, kiongozi wa walio wachache Junet Mohamed alimpongeza Raila kutokana na ujasiri wake akisema, “Unahitaji kuwa na ujasiri mwingi kujitokeza na kusema ninataka kuiwakilisha nchi yangu katika ngazi ya juu zaidi katika Umoja wa Afrika.”
Wabunge walitoa wito wa kuwa na umoja wakati Mkenya yeyote anapogombea wadhifa wa kimataifa.
Ushinde wa Raila uliibua hisia mseto huku baadhi ya Wakenya wakisherehekea kushindwa kwake kwenye wadhifa huo wakati wafuasi wake wakisononeka.
Raila amekuwa Mkenya wa pili kushindwa kutwaa uenyekiti wa AUC baada ya Balozi Amina Mohamed kushindwa na mwenyekiti aliyeondoka siku chache zilizopita Moussa Faki kutoka Chad.