Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria nchini, LSK Faith Odhiambo amejiunga na vuguvugu la Linda Mwananchi.
Hii ilibainika baada ya Odhiambo kupokelewa na viongozi wa vuguvugu hilo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama cha ODM ambaye pia ni Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
“Gwaride kamili kwa Bi. Rais. Karibu kwa Linda Mwananchi,” alisema Sifuna kupitia ukurasa wake wa X.

Odhiambo anajiunga na vuguvugu la Linda Mwananchi ikiwa imesalia miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Haijabainika ni wadhifa gani ambao anamezea mate kuelekea uchaguzi huo, lakini jambo ambalo ni dhahiri ni kwamba kwa kujiunga na Linda Mwananchi, Odhiambo ameazimia kuogolea kwenye bahari ya siasa.
Linda Mwananchi linajumuisha wanaochukuliwa kuwa viongozi waasi wa chama cha ODM.
Wao ni pamoja na Sifuna na mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, ambaye ametangaza azima yake ya kugombea Ugavana wa Nairobi kwenye uchaguzi mkuu ujao.