Rais William Ruto ametaja elimu kuwa uwekezaji muhimu zaidi unaofanywa nchini kwa ajili ya ustawi wake.
Ametaja elimu kuwa ngao muhimu zaidi itakayohakikisha taifa hili linafikia upeo wa maendeleo kama zilivyofanya nchi zilizostawi zaidi kiuchumi na kiviwanda duniani.
“Kati ya zana zote zinazomilikiwa na taifa, elimu ndio muhimu zaidi. Elimu ni daraja kati ya ahadi na uwezaekano. Kati ya umaskini na ustawi. Kati ya kutengwa na kujumuishwa,” alisema Rais Ruto wakati akiongoza taifa kuadhimisha Sikukuu ya Madaraka katika kaunti ya Wajir leo Jumatatu.
“Kinyume cha mwaka 1963, vita vijavyo vya ukombozi wa Kenya vitapiganwa siyo katika viwanja vya kawaida vya vita. Vita hivyo vitashindwa madarasani, maabarani, kwenye karakana, na vituo vya ubunifu.”
Alitoa mfano wa nchi kama vile Korea Kusini aliyosema iliwekeza zaidi katika elimu na kuwa miongoni mwa mataifa yaliyoendelea zaidi duniani.
“Korea Kusini iliwekeza katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu, elimu ya (STEM) na kuwa taifa lililostawi zaidi kiteknolojia duniani. Singapore iliwageuza watu wake kuwa rasilimali kubwa zaidi ya kitaifa. Finland ilijenga uchumi wa maarifa kupitia uwekezaji endelevu katika elimu,” aliongeza Rais Ruto.
Kulinga naye, Kenya imechukua mwelekeo huo, akisema mfumo wa Elimu ya Mtaala wa Umilisi na Mafunzo (CBE) unabadilisha kile ambacho elimu inamaanisha nchini Kenya.
“Unawafanya wanafunzi siyo tu kupita mtihani, bali kufikiria kwa umakinifu, kutatua matatizo, kuwa wabunifu, na kushindana katika jukwaa la kimataifa.”
Alielezea kufurahia kwake kwamba asilimia 52 ya wanafunzi wa Gredi ya 10 wamechagua masomo ya STEM, hatua anayosema itasaidia kuharakisha maendeleo nchini.