Tunawasiliana na Kenya kuhusu ujenzi wa karantini, yasema Marekani

Tom Mathinji
1 Min Read

Siku moja baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kusimamisha kwa muda ujenzi wa kituo cha karantini kuwatibu wagonjwa raia wa Marekani wanaoambukizwa Ebola, Marekani imesema ingali iko na matumaini kwamba swala hilo litashughulikiwa.

Wizara ya Misaada ya Kigeni kupitia ukurasa wa X, ilisema inafahamu kuhusu hatua hiyo ya Mahakama na inawasiliana na utawala wa Kenya kusuluhisha swala hilo.

Tunafahamu kuhusu hatua ya makahakama kuzuia ujenzi wa kituo cha kuwatenga wanaoambukizwa Ebola. Tunawasiliana na utawala wa Kenya kutatua swala hilo,” ilisema taarifa ya wizara hiyo.

Mnamo siku ya Ijumaa, Mahakama Kuu ya Kenya ilisimamisha kwa muda ujenzi wa kituo hicho hadi kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute itakaposikizwa na kuamuliwa.

Habari za ujenzi wa kituo hicho pia hazijapokewa vyema na wakazi wa kaunti ya Laikipia, huku Gavana wa eneo hilo Joshua Irungu akisema wanapinga ujenzi huo.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema kuwa zaidi ya watu 200 wamefariki kutokana na makali ya Ebola, huku zaidi ya 1,000 wakiambukizwa, baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kutokea katika eneo la Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Share This Article