Serikali ya Uganda imepiga marufuku safari za ndege za kuingia na kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC kwa hofu ya msambao wa ugonjwa wa Ebola.
Ingawa Uganda haijarekodi kisa chochote cha Ebola, isipokuwa viwili vya raia wa kigeni, imeamua kuchukua tahadhari ya mapema.
Katibu wa Wizara ya Afya nchini Uganda Dkt.Diana Atwine, amesema changamoto kubwa ya Ebola inatokana na kuendelea kwa biashara baina ya Uganda na DRC.
“Tumesitisha safari zote za ndegekuelekea DRC kutoka Uganda, au za kuingia Uganda kutoka DRC, ndani ya saa 48 na pia tumeweka ulinzi mkali katika mipaka yetu na DRC. Pia tumesimamisha usafiri wote wa kuingia Uganda kutoka DRC, au kutoka Uganda kuingia DRC,” alisema Atwine.
Aidha, Uganda imesitisha safari za barabarani kati yake na DRC na pia usafiri wa majini.
Tahadhari kubwa pia imechukuliwa shuleni na maeneo ya umma.