Mwenyekiti mpya wa NCIC, Makamishna waapishwa

Martin Mwanje
2 Min Read
Mwenyekiti mpya wa NCIC Dkt. Kepha Omae wakati akila kiapo Mei 20, 2026

Mwenyekiti mpya wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) Dkt. Kepha Omae amekula kiapo cha utendaji kazi leo Jumatano asubuhi. 

Dkt. Omae aliapishwa pamoja na makamishna wengine saba wa tume hiyo katika hafla iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome kwenye majengo ya Mahakama ya Juu.

Makamishna hao ni pamoja na Josephine Kirion Eragae, Joseph Nguyo, Jackson Kedogo, na Dkt. Samuel Mwawasi.

Wengine ni Irene Chepoisho, Hassan Billow na Jerusah Mwaathime.

Wote hao watahudumu kwa kipindi cha miaka sita ijayo.

Kwenye hotuba yake, Jaji Koome amewataka kulitumikia taifa kwa uadilifu na kuhakikisha umoja wa Wakenya.

Kwa upande wake, Dkt. Omae ameahidi kufanya kila awezalo pamoja na timu yake kuiunganisha nchi katika ngazi ya kitaifa, kaunti na mashinani kwa ajili ya amani endelevu.

Omae na timu yake wanachukua uongozi wa NCIC wakati ambapo mihemko ya kisiasa imechacha nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Tume hiyo imekuwa ikiwaonya wanasiasa kujiepusha kutoa semi za chuki kwa ajili ya utangamano wa taifa, wito ambao umeonekana kupuuzwa na baadhi ya wanasiasa wakati wakitafuta uungwaji mkono kuelekea uchaguzi huo.

Wengi watasubiri kuona mbinu atakazotumia Dkt. Omae na timu yake kuwatema wanasiasa kama hao, kwani NCIC imeshutumiwa siku zilizopita kwa kukosa kucha za kukabiliana nao isipokuwa kutoa maonyo.

 

 

Share This Article