Wake wa Marais wa mataifa mbalimbali ya Afrika wametoa wito wa mbinu ya pamoja ya kijamii ya kuwalinda watoto katika mazingira ya kidijitali na katika dunia inayozidi kuongozwa na akili mnemba.
Ujumbe huu ulijiri katika hafla ya ngazi ya juu kuhusu Kujenga Mazingira Salama ya Kidijitali kwa Watoto Barani Afrika katika Mkutano wa Africa Forward Summit.
Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa dharura wa serikali, kampuni za teknolojia, wazazi, walimu, na jamii kushirikiana katika kuwalinda watoto mtandaoni.
Mkutano huo, ulioongozwa na Mama wa Taifa Rachel Ruto, uliangazia wajibu unaoongezeka wa kuhakikisha watoto wanasalia salama sasa na hata siku zijazo, huku uchumi wa kidijitali ukiendelea kuzalisha mabilioni ya mapato na kuendesha ubunifu kote barani.
Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Lauriane Darboux épouse Doumbouya mkewe Rais wa Guinea, Marisoa Elisa Berthine mkewe Rais wa Madagascar, Philile Dlamini mkewe kiongozi wa Eswatini na Neema Ngure Nchemba, mke wa Waziri Mkuu wa Tanzania.
Bi. Ruto alisema kuwa teknolojia imebadilisha jamii na kuunganisha dunia kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa awali, hali ambayo imeleta fursa na hatari mpya kwa watoto.
“Dunia kweli imekuwa kijiji cha kimataifa. Lakini wajibu mpya unakuja na mabadiliko hayo. Dunia hiyo hiyo ya kidijitali inayoweza kufungua mustakabali wa mtoto pia inaweza kuuweka katika hatari,” alisema.
Mama wa Taifa alisema kuwa chini ya uongozi wa William Ruto, Kenya inaendelea kupanua upatikanaji wa kidijitali, kuimarisha ubunifu, na kujipanga kuwa mstari wa mbele katika mageuzi ya kidijitali barani Afrika.
“Maendeleo hayapaswi kamwe kupita ulinzi. Tunachojenga si miundombinu tu, tunaunda mazingira ambayo watoto wetu watakulia, kujifunza na kuwa watu wa baadaye,” aliongeza.