Nyota wa kike wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania Zuchu, amekubali msamaha alioombwa na msanii mwenzake Gigy Money, aliowasilisha kupitia akaunti yake ya Instagram.
Gigy Money aliandika ujumbe mrefu akidhihirisha kujuta kuharibu ukaribu wake na Zuchu, akisema kuwa yeye na Zuchu walikuwa zaidi ya ndugu.
Alichapisha video inayomwonyesha akiwa jukwaani akitumbuiza pamoja na Zuchu akamshukuru kwa kuwa kwa maisha yake wakati fulani huku akikiri kwamba yeye ndiye alikosea na kuharibu uhusiano kati yao, bila kutaja alichokifanya.
Natumaini uko salama na unaendelea vizuri. Nimechukua muda kuandika ujumbe huu kwa moyo wa kweli na unyenyekevu.
Msanii huyo alisema kwamba hakutenda makosa hayo makusudi kumuumiza Zuchu au kupunguza thamani ya uhusiano wao, bali alijipata katika hali ya udhaifu kama binadamu.
“Naomba unisamehe kwa dhati kabisa. Siombi ili nirudishe yaliyopita kwa lazima, bali nataka moyo wangu uwe safi mbele yako na mbele ya Mungu,” alielezea Gigy.
Baada ya Ujumbe huo mrefu Zuchu amemjibu Gigy Money akimwambia kuwa ameuona na ameupokea.
“Gigy wangu ndio naona. Maisha ni kujifunza na kuendelea na sisi tumejifunza hatuna budi kuendelea Mwenyezi Mungu ametupa nafasi nyengine ya kua bora zaidi anajua tunapeana faida,” aliandika Zuchu akiongeza kwamba wao ni dada, wanakosana, wanapatana na wanasonga mbele.
“Ninakupenda,” Zuchu alimalizia jibu hilo lake kwa Gigy Money.