Idara ya Mahakama nchini Kenya Ijumaa Mei 8, 2026 ilizindua maonyesho yake ya kwanza ya Vitabu vya Majaji jijini Nairobi, hafla iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Koome alitoa wito wa kuendelezwa kwa uungwaji mkono wa utafiti wa sheria, uandishi, uchapishaji na usambazaji wa maarifa ndani ya idara ya mahakama.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika kituo kikuu cha Huduma za Kitaifa za Maktaba Nchini, KNLS, Jaji Koome alisema kuwa Mahakama inayohamasisha usomaji, utafiti na tafakari huwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutoa haki yenye misingi thabiti na inayowalenga wananchi.
Kaulimbiu ya maonyesho hayo ya vitabu ni “Utafiti wa Kitaaluma wa Majaji na Mchocheo wa Fikra za Kisheria: Uhusiano wa kutegemeana”.
Jaji mkuu alisema mpango huo unaendana na dira ya Mahakama ya Mabadiliko Katika Jamii Kupitia Upatikanaji wa Haki, STAJ, inayolenga kujenga mfumo wa haki unaofikika kwa urahisi, unaoitikia mahitaji ya wananchi na wenye msingi imara wa kielimu.
Koome alibainisha kuwa tafiti za kisheria husaidia kufafanua sheria kwa wananchi na kuwawezesha kuelewa vyema maamuzi ya mahakama na maadili ya kikatiba yanayoongoza majaji.
Alielezea maonyesho hayo ya vitabu kuwa jukwaa la kwanza katika historia ya Mahakama ambapo majaji na maafisa wa mahakama wanaweza kushirikiana na umma kupitia vitabu, kumbukumbu binafsi na mijadala ya kitaaluma nje ya hukumu za mahakamani.
Jaji Smokin Wanjala, Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Mahakama ya Kenya, alisema maonyesho hayo yanadhihirisha dhamira ya Mahakama ya kukuza maendeleo ya kielimu na ushirikishaji wa umma.
Charles Kanjama rais wa chama cha wanasheria nchini LSK, aliahidi kusaidia kuhakikisha machapisho hayo yanawafikia mawakili na wananchi kwa ujumla.