Kamati ya mazingira yamhoji Korir kuhusu kutengwa kwa ardhi ya misitu

Wizara ya Ardhi imetakiwa kuhakikisha kuwa ni wavamizi halali pekee wanaopatiwa vipande vya ardhi

Marion Bosire
2 Min Read
Vincent Musyoka, Mwenyekiti, Kamati ya bunge la taifa kuhusu Mazingira, Misitu na Madini

Kamati ya bunge la taifa kuhusu Mazingira, Misitu na Madini imeitaka Wizara ya Ardhi kuhakikisha kuwa ni wavamizi halali pekee wanaopatiwa vipande vya ardhi.

Hili litawezekana tu iwapo pendekezo la kuondoa sehemu za ardhi ya hifadhi za misitu na kuhalalisha umiliki wa ardhi hiyo litapitishwa.

Katika kikao cha leo kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Vincent Musyoka, kamati ilitaka kujua vigezo vilivyotumiwa na wizara kubaini wakaazi wa sasa wa maeneo hayo, orodha ya wamiliki halali, kama kumekuwa na uhamisho wa umiliki kwa miaka mingi, na iwapo Tume ya Taifa ya Ardhi ilithibitisha haki za umiliki wa vipande vya ardhi vinavyozingatiwa.

“Kamati hii imeombwa na Baraza la Mawaziri kuachilia ardhi inayomilikiwa na Huduma ya Misitu Kenya ili kuwapa makazi wavamizi ambao, kwa tathmini yetu, tayari wanaishi katika maeneo hayo,” alisema Musyoka.

Kikao hicho kilitokana na matokeo ya ukaguzi uliofanywa na kamati katika maeneo ya Manzini ndani ya Msitu wa Turbo, Chepyuk katika Msitu wa Mlima Elgon, pamoja na maeneo ya Shiru na Shaviringa ndani ya Msitu wa Kakamega.

Vipande vya ardhi vilivyotengwa na Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuondolewa chini ya hifadhi vina watu ambao wameishi humo kwa zaidi ya miaka arobaini, baadhi yao wakidai kuwa waliondolewa katika makazi yao ya awali na serikali.

Wakieleza wasiwasi kuwa orodha inayodaiwa kuwa ya wakaazi na wamiliki wa maeneo hayo imezua maswali miongoni mwa viongozi wa jamii, wabunge walimtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nixon Korir, kuhakikisha kuwa watu wanaotambuliwa kama wanaoweza kupewa hati miliki ndio wamiliki halali, wakionya kuhusu uwezekano wa kutokuelewana kati ya serikali na jamii.

“Ni muhimu kama kamati tusipendekeze kuondolewa kwa hifadhi ya misitu bila kuwa na mwongozo wazi kuhusu nani watakaonufaika,” alisema Mwenyekiti huyo.

Kamati hiyo imemwelekeza Katibu kushirikiana na Tume ya Taifa ya Ardhi, viongozi wa jamii, utawala wa maeneo husika pamoja na wavamizi wenyewe kubaini idadi halisi ya wakaazi wa maeneo hayo na kuandaa kanzidata ya kuaminika itakayotumika katika ugawaji wa ardhi iwapo pendekezo la kuhalalisha umiliki litapitishwa.

 

Share This Article