Maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, wamekamata washukiwa wawili na kufanikiwa kukamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya katika operesheni maalum iliyofanyika katika kituo cha biashara cha Suswa.
Washukiwa hao waliotambuliwa kama Elizabeth Njoki Mukiri na Alfa Mukiri, walikamatwa kufuatia taarifa za kijasusi zilizowaunganisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Operesheni hiyo ilitekelezwa na maafisa wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya kutoka Nakuru na Narok.
Wakati wa kukamatwa kwao, maafisa walinasa bangi kilo 6 na misokoto 240, lita 30 za chang’aa, katoni 6 za pombe haramu aina ya second generation, pamoja na pakiti 20 za karatasi za kuvutia sigara.
Vitu hivyo vinashikiliwa kama ushahidi.
Washukiwa walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Narok ambapo wanashughulikiwa wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Mamlaka zinasema operesheni hiyo inaonesha juhudi zinazoendelea katika vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya na kuthibitisha dhamira ya vyombo vya usalama kulinda jamii.
Wananchi wanahimizwa kuripoti shughuli zozote za kutiliwa shaka kupitia njia za siri zilizotolewa na DCI.