Mwili wa mwanafunzi wapatikana mshukiwa wa mauaji yake akikamatwa Kisumu

Mwanafunzi huyo wa chuo cha RIAT alikuwa ameripotiwa kutoweka awali

Marion Bosire
2 Min Read

Maafisa wa upelelezi huko Kisumu Magharibi, kwa ushirikiano na maafisa wa kituo cha polisi cha Maseno na wale kutoka kituo cha polisi cha Riat, wamefanikiwa kuupata mwili uliokuwa umeanza kuoza wa mwanafunzi wa kike wa umri wa miaka 21.

Mwanafunzi huyo wa chuo cha RIAT alikuwa ameripotiwa kutoweka awali kabla ya mwili wake kupatikana kwenye msitu wa RIAT.

Mwili huo uliokuwa na majeraha ya kuchomwa kisu na ulipatikana baada ya mshukiwa mkuu Steven Coleman Okoth, kukamatwa.

Okoth anadaiwa kupanga ubakaji wa kundi, mateso na kutoweka kwake baadaye, tukio la kutisha lililotokea katika eneo la Milimani, Kisumu usiku wa tarehe 5 Aprili 2026.

Dada mkubwa wa mwathiriwa alijawa wasiwasi baada ya kushindwa kuwasiliana naye, hofu yake ikithibitishwa usiku wa manane alipopokea ujumbe wa kushtua.

Ilibainika kuwa mwendazake alishawishiwa kwenda kunywa pombe na wanaume wawili ambao ni wenzake katika chuo hicho cha RIAT, hali iliyomfanya apoteze fahamu.

Akiwa katika hali hiyo dhaifu, alibakwa na baadaye kuachwa kichakani akiwa katika hali mbaya na simu yake ikazimika kabla hajapata msaada.

Wakichukua hatua haraka kufuatia taarifa hiyo ya kuhuzunisha, wapelelezi kutoka Kitengo cha Kisumu Magharibi walianzisha uchunguzi wa kina.

Kwa kutumia ushahidi wa kitaalamu wa kisayansi, walifuatilia eneo la mwisho alipoonekana mwathiriwa katika eneo la Milimani karibu na afisi za Kenya Wildlife Service lakini icha ya msako mkali, hawakufanikiwa kumpata.

Uchunguzi ulioendelea kwa umakini ulitoa mwanga zaidi pale mshukiwa mmoja alipotambuliwa na kukamatwa. Inasemekana alikuwa mpenzi wa zamani wa mwathiriwa na alionekana akiwa naye akiwa amewekewa dawa kali jioni hiyo.

Uchunguzi zaidi ulifichua kuwa mshukiwa huyo alikuwa ametoa vitisho kwa mwathiriwa kwa miezi miwili iliyopita na mara kwa mara alitembelea makazi yake RIAT akimtafuta.

Wakati wa kukamatwa mshukiwa alipatikana na vielelezo muhimu vinavyotumika kama ushahidi, ambavyo wapelelezi wamekuwa wakitumia katika kutafuta mwanafunzi aliyekuwa ametoweka pamoja na washukiwa wengine.

Coleman Steve Okoth kwa sasa anasubiri kufikishwa mahakamani huku msako wa kuwatafuta washirika wake ukiendelea.

Share This Article