Papa Leo XIV kuanza ziara yake ya Afrika leo

Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki atazuru Algeria, Cameroon, Angola na Equatorial Guinea.

Marion Bosire
2 Min Read
Pope Leo XIV

Papa Leo XIV anatarajiwa kuanza ziara yake ya siku 11 ya Afrika, leo ambayo ni ziara yake ya kwanza kabisa katika Bara hili.

Ziara hiyo itakayofikia kikomo Aprili 23, 2026 itakuwa ndefu kabisa kwake na itajumuisha mataifa ya Algeria, Cameroon, Angola na Equatorial Guinea.

Akiwa kwenye safari hiyo, kiongozi huyo wa kanisa Katoliki ulimwenguni na kiongozi wa nchi ndogo ya Vatican atatumia lugha za kingereza, kifaransa, kireno na kihispania.

Kulingana na Mkurugenzi wa afisi ya habari ya Vatican Matteo Bruni, Papa Leo ataangazia amani, uhamiaji, mazingira, vijana na familia katika safari hiyo.

Papa Leo ndiye kiongozi wa kwanza wa kanisa Katoliki ulimwenguni kuzuru Algeria na atazuru nchi hizo nyingine tatu kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu tangu zilipotembelewa na Papa.

Akiwa nchini Algeria Papa atarejelea urithi wa Mtakatifu Augustine na uwepo wa ukristo Afrika Kaskazini, pamoja na mazungumzo na ulimwengu wa Kiislamu na suala la uhamiaji.

Huko Cameroon, nchi inayodhaniwa kuwa Afrika ndogo kutokana na utofauti wa ardhi yake, tamaduni na lugha, Papa anatarajiwa kujadili mada zinazohusiana na amani, kuishi kwa pamoja, vijana na maendeleo kamili ya binadamu.

Angola kipaumbele kitakuwa juu ya jukumu la vijana, rasilimali za asili na binadamu na athari za ufisadi na historia ya kikoloni.

Hatimaye nchini Equatorial Guinea Papa Leo ataangazia sana tamaduni na elimu, pamoja na jukumu la Kanisa katika kukuza amani katika eneo lenye rasilimali nyingi.

Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki ataandamana na wawakilishi wa idara mbali mbali pamoja na maaskofu kadhaa kutoka Afrika.

Share This Article