Aliyeua watoto wa chekechea Kampala ahukumiwa kifo

Alivamia watoto wachanga katika kituo cha Ggaba Aprili 2, 2026, na kuua wanne kwa kuwadunga kisu.

Marion Bosire
2 Min Read
Christopher Okello Onyum

Mahakama Kuu ya Uganda imemhukumu Christopher Okello Onyum, mshtakiwa wa mauaji ya watoto wa kituo cha utunzaji wa watoto cha Ggaba jijini Kampala, adhabu ya kifo.

Haya yanajiri baada ya mahakama hiyo kumpata na hatia ya makosa manne ya mauaji ya kikatili ya watoto wanne na hivyo kufunga kesi hiyo ya jinai ya kutisha sana.

Jaji Alice Komuhangi Khauka alitoa hukumu hiyo leo Alhamisi Aprili 30, 2026, jioni akisema kwamba kesi hiyo iliafikia kiwango cha nadra sana kinachostahili adhabu ya kifo.

Katika maelezo yake ya hukumu, Jaji Khauka alisema alizingatia kwa makini ombi la kupunguza adhabu lililowasilishwa na upande wa utetezi na mambo mazito yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka.

Jaji alibainisha kwamba ingawa upande wa utetezi ulidai kuwa Okello anatoka katika familia yenye changamoto, uzito wa uhalifu aliotekeleza, ulizidi ombi hilo.

Alisema kwamba mahakama ilipata ushahidi kuwa uhalifu huo ulipangwa kwa makini na kutekelezwa kwa ustadi, ambapo Okello aliwashambulia watoto wasio na hatia na wasio na uwezo wa kujilinda, ambao hutegemea ulinzi wa watu wazima.

Mwenendo wa mshitakiwa ulitajwa pia mahakamani wakati wa kutoa hukumu, jaji akibainisha kwamba Okello hakuonyesha majuto.

Jaji alihitimisha kwa kusema kwamba hakuna adhabu nyingine nyepesi inayoweza kutimiza haki, akikubaliana na kauli ya upande wa mashtaka ambao umeridhia hukumu hiyo.

Share This Article