Gloria Orwoba akamatwa nje ya majengo ya Bunge

Alifika langoni huko bungeni akitaka kuingia kazini kama kawaida

Marion Bosire
2 Min Read
Seneta wa zamani Gloria Orwoba akikamatwa nje ya bunge mwaka jana

Aliyekuwa Seneta Mteule Gloria Orwoba amekamatwa muda mfupi uliopita nje ya majengo ya bunge kutokana na kile kinachodaiwa kuwa hatua yake ya kuwa kizuizi katika lango la bunge.

Video inayoonyesha maafisa kadhaa wa polisi wa kike wakiwa wamembeba Orwoba kuelekea kwenye kituo cha polisi cha bunge ilichapishwa kwenye akaunti yake ya Facebook.

Maelezo chini ya video hiyo ni kama yafuatavyo, “Seneta Orwoba amefungiwa katika seli za Kituo cha Polisi cha Bunge, amepigwa na sasa wanapanga ni kosa gani watamshtaki nalo. Seneti iliagizwa na Mahakama Kuu kumrejesha kazini, lakini Spika wa Seneti pamoja na Karani wa Seneti—ambaye muda wa mkataba wake umeisha na anaendelea kufanya kazi kinyume cha sheria—sasa wanapanga mashtaka ya kubuni. Gari lake rasmi limevutwa kinyume cha sheria hadi mahali pasipojulikana.”

Haya yanajiri yapata miezi minane baada ya tukio sawia ambapo Seneta huyo wa zamani alifika nje ya bunge tayari kuingia kazini baada ya jopo la kusuluhisha mizozo ya vyama vya kisiasa kubatilisha kuondolewa kwake bungeni.

Katika video nyingine ya leo kabla ya purukushani, Orwoba anasikika akiambia maafisa wa usalama waliokuwepo langoni kwamba yeye ndiye anastahili kuwashtaki kwa kumzuia kuingia kazini akiwa amejihami na nakala za maamuzi ya jopo hilo na Mahakama Kuu.

Uamuzi wa jopo hilo wa kubatilisha kuondolewa kwa Orwoba ni wa Agosti 20, 2025, na hivi maajuzi hususan Aprili 14, 2026, Mahakama Kuu ilikubaliana na uamuzi wa jopo hilo na kuagiza chama cha UDA kufuata uamuzi wa jopo lililoelekeza kwamba arejeshwe katika wadhifa wake.

Share This Article