Wanachama wa kamati ya bunge la taifa kuhusu biashara, viwanda na vyama vya ushirika, wamekatalia mbali mpango wa idara ya uwekezaji kugawa upya shilingi milioni 200 ilizokuwa imetengea halmashauri ya eneo la kutayarisha bidhaa za kuuzwa nje ya nchi (EPZA).
Wakiongozwa na mwenyekiti wao ambaye ni mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya, wanachama hao walilaumu idara hiyo kwa kutekeleza hatua hiyo bila kushairiana na kamati hiyo.
Katibu wa idara ya uwekezaji Hassan Abubukar alipokuwa akiwataarifu wanachama hao kuhusu miradi inayotekelezwa na idara yake, alikiri kutekeleza hatua hiyo baada ya ya kushauriana na hazinakuu.
Katibu Abubakar aliwaambia wabunge hao wa bunge la taifa kwamba aliiandikia hazina kuu akitaka idhini ya kusambaza upya shilingi hizo milioni 200 zilizokuwa zimetengewa EPZA katika bajeti ya kwanza ya ziada ya mwaka 2024/2025.
Kulingana na Abubakar, katika barua yake kwa hazina kuu, alipendekeza shilingi milioni 50 zisalie EPZA , huku shilingi milioni 100 zisamazwe katika halmashauri ya uwekezaji ya Kenya na na shilingi milioni 50 kwa maeneo maalum ya kiuchumi (SEZA).
Matamshi yake yaliibua hisia kali kutoka kwa wabunge hao, huku Gakuya na naibu wake Marianne Kitanymbunge wa Aldai, wakidokeza ni bunge tu iliyo na mamlaka ya kutenga upya fedha.
“Ni bunge tu iliyo na mamlaka ya kugawa upya fedha kwa mashirika ya umma, ulipaswa kutafuta ushauri wa kamati hii kwanza,” alisema Gakuya.
Kwa upande wake Kitany alieleza kuwa iwapo idara za serikali zilihitaji fedha, zingepaswa kufuata utaratibu ufaao.
“Iwapo kuna haja kwa mashirika ya umma kuhitaji fedha, yanapaswa kutafuta idhini kutoka kwa bunge,” alieleza Kitany.
Hata hivyo katibu huyo alikiri kuwepo kwa dosari, alikini alidokeza kuwa hatua hiyo ilifaidi mashirika hayo ya serikali.