Wizara ya Afya imetia saini mkataba na serikali za kaunti kufanikisha utekelezaji wa Taifa Care, kwa lengo la kuafikia Huduma za Afya kwa Wote (UHC).
Katika mkutano huo ulioongozwa kwa pamoja na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, wizara ya Afya na serikali za kaunti zilikubaliana kutatua changamoto zinazokumba sekta ya afya, hususan kuimarisha huduma za afya kwa wote UHC.
Mkataba huo ulijumuisha:
- Usambazaji wa tarakilishi 74,000 kwa vituo vya afya katika kaunti zote 47.
- Kuhakikisha vituo vyote vya Afya vinatumia mfumo wa dijitali.
- Utoaji mafunzo za dijitali kwa wahudumu wote wa afya.
- Kubuni mfumo thabiti wa ubadilishanaji habari kuhusu afya.
- Kuzindua mfumo wa kielektroniki kuhusu maswala ya bima.
- Kuzindua mfumo wa kidijitali wa maelezo kuhusu usambazaji wa dawa kuhakikisha uwajibikaji.
- Kuwa na huduma ya kitaifa kuhusu huduma za dharura.
- Kubuni mfumo utakaowezesha wananchi kufuatilia habari zao za matibabu kupitia mtandao.
Waziri Duale alikariri kujitolea kwa wizara yake kuimarisha ushirikiano na umma, sekta ya kibinafsi na wadau wengine katika kuhakikisha huduma za afya za ubora wa hali ya juu.
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na katibu wa huduma za afya Dkt. Ouma Oluga, mwenzake wa Afya ya Umma Mary Muthoni na Mkurugenzi Mkuu wa huduma za Afya Dkt. Patrick Amoth