Waziri Ndung’u asema vituo vya dijitali vinaweza kuwa vya uvumbuzi na ujumuishaji

Waziri huyo alikuwa akizungumza kwenye hafla ya kuzindua kituo cha dijitali huko Kakamega, ambapo alisisitiza kwamba vituo hivyo sio vya upatikanaji wa mtandao tu bali pia ni majukwaa ya vijana kuwezeshwa, kutumia ubunifu wao na kuziba pengo kwa walemavu.

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Dkt. Margaret Nyambura Ndung’u amesema kwamba vituo vya dijitali ni muhimu sana katika kuwezesha uvumbuzi na ujumuishaji nchini Kenya.

Akizungumza kwenye hafla ya kuzindua kituo cha dijitali huko Kakamega, Waziri huyo alisisitiza kwamba vituo hivyo sio vya upatikanaji wa mtandao tu bali pia ni majukwaa ya vijana kuwezeshwa, kutumia ubunifu wao na kuziba pengo kwa walemavu.

Dkt. Ndung’u aliangazia athari za vituo dijitali ambavyo vinatoa vifaa muhimu, ujuzi wa kidijitali na mtandao wa kasi ya juu kwa jamii za maeneo ambako vimewekwa.

Kulingana naye, vinasaidia kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma katika masuala ya uchumi dijitali huku akifichua mipango ya kuvipanua hata zaidi.

Upanuzi huo utajumuisha vifaa vya kuunda maudhui ya kuchapisha mitandaoni ambavyo vitasaidia vijana kujipatia kipato kutokana na uchumi dijitali.

“Vituo hivi ni muhimu katika kuwapa vijana uwezo na kuwawezesha kuvumbua, kujipatia riziki na kuunganishwa na soko la ulimwengu,” alisema Dkt. Ndung’u katika hotuba yake.

Waziri alitambua pia ufanisi wa kituo cha kidijitali cha Kakamega ambacho kimeongeza upatikanaji wa huduma za mtandao kutoka asilimia 20 hadi asilimia 80 katika vyuo vya mafunzo ya kiufundi.

Alithibitisha kujitolea kwa serikali kuhakikisha vituo vya kidijitali vinakuwa nguzo katika safari ya mabadiliko ya kidijitali nchini, kwa usaidizi wa washirika kama kampuni ya Huawei na Chuo Kikuu cha Strathmore.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *