Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Alfred Mutua amelishukuru Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC kwa kuidhinisha kupelekwa kwa maafisa wa polisi nchini Haiti.
Kikosi hicho cha kimataifa kitaongozwa na Kenya.
Waziri Mutua anasema hiyo ni fursa nzuri ya kusaidia watu wa taifa la Haiti ambao wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa usalama kutokana na wingi wa magenge ya wahalifu yaliyojihami kwa silaha.
Mutua pia amewashukuru wote waliochangia katika kuboresha azimio hilo la kusaidia kikosi cha polisi cha Haiti.
Anaomba washirika wote wa kimataifa waunde kikosi bora cha kimataifa ndani ya muda mfupi na ambacho kitakita kambi nchini Haiti kwa nia ya kubadilisha maisha ya watu wa nchi hiyo.
Anasema idhini hiyo sio tu ya kurejesha amani na usalama bali pia inalenga kujenga tena taifa la Haiti, kuboresha siasa zake, kuboresha ukuaji wake kiuchumi na kuhakikisha uthabiti wa kijamii.
“Ni mwanzo mpya kwa kina baba, kina mama na watoto wa Haiti,” aliandika Waziri Mutua akiongeza kwamba hatua hii inalenga kufanikisha Haiti huku ikiimarisha amani na usalama ulimwenguni.
Wanachama wa UNSC walipiga kura jana Oktoba 2, 2023 kuidhinisha azimio hilo ambalo lilianzishwa na Marekani na Ecuador.