Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen amesisitiza kuwa maafisa wa usalama watafanya kila wawezalo kukabiliana na uhuni na vurugu za kisiasa nchini.
Murkomen amesema hadi kufikia sasa, washukiwa 20 tayari wamekamatwa na watafikishwa mahakamani kuhusiana na vurugu zilizotokea jana Jumapili katika maeneo ya Kisumu na Nyahururu.
“Hebu tusianze kutoa madai ni kana kwamba hakuna chochote kinachofanywa na polisi kuhusu hili. Watu zaidi ya 20 wamekamatwa kuhusiana na matukio ya jana,” alisema Murkomen.
Waziri akiitaka idara ya mahakama kutoa adhabu kali kwa washukiwa ili kuwakatisha tamaa watu wengine kujihusisha na vitendo vya kihuni.
“Ni lazima tufanye kazi na Idara ya Mahakama. Wakati tunapowafikisha washukiwa hawa mahakamani, mahakama zinapaswa kuchukua hatua kali dhidi yao kuendana na makosa yao.”
Alidokeza kuwa ametoa agizo kali kwa Inspekta Mkuu wa Polisi kuongeza operesheni ya usalama dhidi ya wahuni na wafadhili wao bila kujali mirengo yao ya kisiasa au hadhi yao katika jamii.
Murkomen kadhalika alitoa onyo kali kwa viongozi wa kisiasa wanaochochea vurugu na migawanyiko ya kikabila na hivyo kutishia usalama wa kitaifa akisema watakamatwa.
“Kuna watu wanaosema tunapaswa kuwakamata wanasiasa. Tutawakamata. Tutakapopata ushahidi wa kutosha, hakika tutawakamata”.
Waziri huyo aliwahakikishia wakazi wa Ol Kalou usalama wa kutosha wakati wa uchaguzi mdogo utakaoandaliwa katika eneo hilo Alhamisi hii.
Aliyasema hayo katika eneo la Lokori, kaunti ya Turkana alipohudhuria hafla ya mazishi.