Waziri Murkomen aagiza kufanywa ukarabati katika viwanja vya ndege

Tom Mathinji
2 Min Read

Waziri wa uchukuzi na barabara Kipchumba Murkomen, ameagiza kuwekwa kwa paa mpya  katika maeneo yote ya wasafiri  katika uwanja wa ndege wa Kimataifa Jomo Kenyatta (JKIA).

Kupitia kwa mtandao wa X, Murkomen pia aliagiza kuboreshwa kwa hali ya usafi,maeneo ya kuingiza hewa na kuongezwa kwa mwangaza.

Waziri huyo alitoa maagizo hayo baada ya kupokea ripoti kutoka kamati ya kiufundi iliyobuniwa kutathmimi hali katika viwanja vya ndege vya Jomo Kenyatta, Moi na Wilson na kutoa mapendekezo ya kuviboresha.

Aidha Waziri Murkomen aliagiza kujengwa kwa mabomba ya kupitishia maji na njia za wanaotembea kwa miguu katika uwanja huo wa ndege wa Jomo Kenyatta.

Na katika uwanja wa ndege wa Moi, Waziri huyo aliagiza kukarabatiwa kwa barabara, mabomba ya kupitisha maji, kuwekwa alama za barabarani pamoja na kuwekwa kwa vifaa vya uchunguzi.

Vile vile aliagiza kuondolewa kwa kebo za chini ya ardhi za zamani na kuwekwa mpya, vifaa vya uchunguzi na paa zilizochakaa katika uwanja wa ndege wa Moi.

Katika uwanja wa ndege wa Wilson, Waziri huyo aliagiza kutengwa kwa eneo la kuwabeba na kiwashukisha abiria, vifaa vya uchunguzi na kujengwa kwa mabomba ya kupitisha maji.

Hivi majuzi paa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta zilikuwa zikivuja huku taifa hili likishihudia mvua za El Nino.

” Sisi kama serikali tuko tayari kushirikiana na wadau wote kuboresha viwanja vyeti vya ndege,” alisema Waziri Murkomen.

Share This Article