Waziri mkuu wa Australia ameomba msamaha wa kitaifa kwa manusara wa kashfa ya dawa ya Thalidomide na familia zao.
Hayo yamejiri yapata miaka 60 tangu dawa hiyo ya kudhibiti matatizo ya nyakati za asubuhi kwa waja-wazito kuanza kusababisha kasoro kwa watoto waliozaliwa duniani kote.
Anthony Albanese aliambia bunge kwamba msamaha huo umetambua kile alichotaja kuwa tukio baya zaidi katika historia ya sekta ya matibabu nchini humo.
Ndio mara ya kwanza kwa serikali ya nchi hiyo kukubali makosa yake kwenye kashfa hiyo. Idadi kamili ya waathiriwa nchini Australia haujulikani japo watu 140 wamejisajili kwa mpango wa usaidizi wa kifedha tangu mwaka wa 2020.
Mnamo mwaka wa 2019, ripoti ilibaini kwamba asilimia 20 ya visa vya Thalidomide ingeepukwa ikiwa viongozi wangemakinika haraka iwwezekanavyo.
Dawa hiyo iliyotengenezwa nchini Ujerumani mnamo miaka ya hamsini, ilitumika kulalisha wagonjwa ila baadaye ilisambazwa kote ulimwenguni kama dawa ya kukabili matatizo ya asubuhi kwa mama wajawazioto.
Na huku matumizi yake yakizidi ndivyo visa vya kasoro za kimaumbile kwa watoto waliozaliwa vilivyozidi kuripotiwa.