Watu zaidi ya 700,000 wameandikishwa katika zoezi linaloendelea la usajili wa watu wanaonufaika na Mpango wa Inua Jamii.
Zoezi hilo ambalo limeingia wiki ya pili linaendeshwa na Wizara ya Leba inayosimamiwa na Florence Bore.
Waziri Bore alitembelea maeneo bunge ya Moiben, Kesses na Turbo leo Jumatano kupigia darubini uendeshaji wa zoezi hilo linalowalenga wazee, watoto mayatima, watoto wasiojiweza katika jamii na watu wanaoishi na ulemavu.
“Idadi ya waliosajiliwa kufikia Septemba 12, 2023 ni watu 718, 103. Ulinzi wa jamii unahusisha kuwakinga watu wasiojiweza katika jamii kwa lengo la kuimarisha vyanzo vyao vya kujipatia kipato,” alisema Waziri Bore wakati akizuru maeneo bunge hayo yaliyopo kaunti ya Uasin Gishu.
Serikali inadhamiria kuongeza idadi ya watu wanaonufaika chini ya mpango wa Inua Jamii kutoka idadi ya sasa ya watu milioni 1.2 hadi milioni 2.5.