Jamaa aliyejichoma nje ya bunge la Uganda afariki

Alikuwa akilalamikia kutelekezwa na chama cha NRM

Marion Bosire
1 Min Read

Benjamin Agaba, mfuasi sugu wa chama tawala nchini Uganda NRM, ambaye alijichoma moto nje ya bunge la nchi hiyo mwezi uliopita wa Februari ameaga dunia.

Agaba anaripotiwa kukata roho katika hospitali ya Kiruddu ambako amekuwa akipokea matibabu kufuatia kitendo cha kujichoma cha Februari 26.

Naibu msemaji wa polisi katika eneo la Kampala Metropolitan Luke Owoyesigyire alisema kwamba Agaba alionekana kwenye barabara ya bunge siku hiyo akiwa amebeba chupa.

Chupa hiyo inaaminika kuwa ilikuwa imebeba Petroli ambayo alijimiminia na kisha kuwasha kiberiti.

Owoyesigyire katika taarifa yake alielezea kwamba walinzi wa bunge walichukua hatua za haraka kumsaidia ambapo walimmiminia maji na hivyo kuzima moto huo.

Agaba alipelekwa kwanza katika hospitali ya Mulago kwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa ile ya Kiruddu.

Huku polisi wakiendelea kuchunguza kilichosababisha Agaba ajichome, ripoti zinaashiria kwamba alikuwa amelaumu chama tawala cha NRM kwa kumtelekeza.

Alisema mali yake iliharibiwa na wafuasi wa chama cha upinzani cha NUP na hivyo kusababisha babake mzazi kupoteza makazi.

Jamaa huyo alidai kwamba alikuwa ametafuta usaidizi kwa afisi za chama cha NRM kwa zaidi ya mwaka mmoja lakini hakupata.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *