Watu watano wamethibitishwa kufariki katika mafuriko kufuatia mvua kubwa katika jiji kuu la Uganda Kampala. Miili ya watatu ilipatikana katika eneo la Kinawataka na juhudi za utambuzi zinaendelea.
Watoto wawili mmoja wa umri wa miaka mitatu na mwingine wa miezi 11 walikufa maji nyumbani kwao katika eneo la Mulimira huko Bukoto.
Mama ya watoto hao alikuwa amewafungia kwenye nyumba yao na kwenda kazini. Alikamatwa na maafisa wa polisi kwa tuhuma za uzembe huku majirani wakielezea kwamba ni mazoea yake kufungia watoto kwa nyumba.
Msemaji wa polisi katika eneo la Kampala Luke Owoyesigyire, alithibitisha vifo hivyo na kuhakikishia umma kwamba maafisa wapo nyanjani kutathmini hali na kutoa usaidizi.
“Tunaomba watu watahadhari wakati huu wa mvua nyingi ili kuepuka ajali zaidi.” alisema Owoyesigyire.
Maafisa wa polisi wa jiji la Kampala kwa ushirikiano na idara ya zimamoto wanaendelea kushughulikia miito inayopokelewa ya usaidizi katika sehemu kadhaa zilizofurika jijini Kampala.
Mvua hiyo ilisababisha ajali za magari, wanaotembea kwa miguu kusombwa na maji ya mafuriko na uharibifu mkubwa wa mali.
Wakazi wa maeneo yaliyoathirika wameshauriwa kutotembea tembea ovyo iwapo hawalazimiki huku waendesha boda boda wakishauriwa kusubiri hadi viwango vya maji vipungue kabla ya kuendeleza safari zao.
Miili ya wahasiriwa ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Mulago ambapo itafanyiwa uchunguzi.