Washukiwa wa ujambazi wakamatwa kaunti ya Kwale

Tom Mathinji
2 Min Read
Washukiwa 12 wa ujambazi wakamatwa Pwani.

Katika juhudi za kukabiliana na magenge ya wahalifu ambayo yamewakosesha usingizi wakazi wa Pwani, maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa 12, wanaoaminika kuwa wanachama wa magenge ya wahalifu.

Kulingana na idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, washukiwa hao waliokamatwa wanatuhumiwa kuwashambulia na kuwaibia wakazi na wafanyabiashara katika kaunti ya Kwale na viunga vyake, wakiwa wamejihami kwa mapanga na visu.

Washukiwa hao waliokamatwa katika operesheni ya polisi ni;  Rajab Hamisi Dele, Aliphan Yusuf, Soud Mwariga Abdalla, Isaya Wanyama Simiyu, Eagan Jason Ndiwa, Ndaro Mzungu Ndaro, Saidi Ali Tengeza, Ali Abdalla Mwagula, Athman Ramadhan Mwachibuyu, Suleiman Mohammed Suleiman, Gilbert Obiero, na Emmanuel Erri.

Kupitia ukurasa wake wa X, DCI ilisema kuwa baada ya kuwahoji washukiwa hao, walifanikiwa kufahamishwa kuhusu wanachama wengine wa magenge ya wahalifu na operesheni zaidi imezinduliwa kuwatia nguvuni.

Eneo la Pwani katika siku za hivi karibuni imeshuhudia kuibuka kwa magenge ya wahalifu ambao huwashambuliwa waathiriwa wakiwa na mapanga na kuwaibia mali yao. Wanaokiuka maagizo yao hujeruhiwa vibaya kutumia silaha hizo.

Kamanda wa polisi eneo la Pwani Ali Nuno, amewaonya wahalifu hao kwamba watachukuliwa hatua kali iwapo hawatasitisha uhuni wao.

Hata hivyo baadhi ya vijana waliokuwa wanachama wa magenge hayo, walijisalimisha na kusema kuwa wamerekebisha tabia.

Washukiwa hao 12, wanasubiri kufikishwa mahakamani.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article