Washukiwa 2 wakamatwa, bangi ya mamilioni ya pesa yanaswa Mombasa

Martin Mwanje
1 Min Read

Washukiwa wawili wa ulanguzi wa bangi wamenaswa katika operesheni ya pamoja iliyofanywa na makachero kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Moi na Kitengo cha Kukabiliana na Mihadarati (ANU) mjini Mombasa. 

Chrispin Oduor Owino na Caleb Otieno Agolo walikamatwa na bangi hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 13 baada ya umma kuwataarifu maafisa hao kuhusiana na usafirishaji wa bangi hiyo.

Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasema gari walimokuwa wakisafirishia bangi hiyo aina ya Toyota Noah KBQ 605K lilisimamishwa katika daraja la Mariakani baada ya maafisa hao kukita kambi hapo kwa muda.

“Ndani ya gari, maafisa waligundua uwepo wa misokoto 26 ya bangi. Ukaguzi zaidi ulibaini kuwepo kwa nambari nyingine ya usajili wa gari KBW 664P iliyokuwa imefichwa chini ya kiti cha dereva,” imesema DCI katika taarifa.

Washukiwa hao walipelekwa katika kituo cha polisi cha Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Moi ili kuhojiwa zaidi na bidhaa hiyo kuthibitishwa kuwa bangi ya kilo 456 baada ya kufanyiwa uchunguzi na mkemia wa serikali.

Washukiwa wanazuiliwa wakisubiri kufikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka dhidi yao.

Share This Article