AFC Leopards maarufu kama chui,Kariobangi Sharks na Sofapaka AKA Batoto Ba Mungu, wamepoteza mechi za ligi kuu Kenya FKF za raundi ya kumi zilizochezwa Jumamosi katika nyuga mbalimbali.
Katika uwanja wa Kasarani Chui wameambulia kichapo cha mabao 3-2 dhidi ya Nairobi City Stars,Vincent Owino,Samuel Kapen na Robinson Asenwa wakipachika moja kila moja kwa City huku Brian Yakhama na Victor Otieno wakifunga magoli ya kufutia machozi kwa Ingwe.
Ugani Sudi Nzoia Sugar wamerejelea tambo za ushindi baada ya kuwanyofoa Kariobangi Sharks goli moja kwa sifuri,Emmanuel Osoro akiwafungia wenyeji bao pekee na la ushindi katika dakika ya 90.
Katika uwanja wa kaunti ya Machakos wageni Talanta FC wamekosa adabu za mgeni walipoidhalilisha Sofapaka kwa kichapo cha tatu bila.