Wanamuziki kadhaa wa Kenya wanatarajiwa kuandaa tamasha za kusherehekea muda wao katika tasnia ya muziki katika siku chache zijazo.
Mashabiki wa wasanii husika wanasubiri kwa hamu maonyesho mazuri kusherehekea miaka ya vibao vilivyotamba, mchango wao katika utamaduni, na maonyesho ya moja kwa moja yaliyowavutia wengi.
Nadia Mukami anafungua orodha hiyo fupi ambapo anaandaa tamasha ya kuadhimisha miaka 10 tangu aanze safari yake katika tasnia ya muziki, Agosti Mosi, 2026, ndani ya Mass House, Nairobi.
Wasanii alioorodhesha watakaotumbuiza siku hiyo ni pamoja na Otile Brown, Bahati, Sanaipei Tande, Nyota ndogo, Iyanii, Masauti, Fena Menal, Breeder, Maandy, Ssaru, Dufla Diligon, Fayhermoh, Vijana Barubaru na Jaysoul.
David Mathenge maarufu kama Nameless naye anapanga tamasha sawia ya kuadhimisha miaka 25 katika tasnia, hafla itakayofanyika siku mbili katika uwanja wa Carnivore Nairobi.
Nameless anaendelea kuunda orodha ya watakaotumbiza Jumamosi na Jumapili Agosti 15 na 16, 2026, akimtaja Wyre kuwa mmoja wao.
Wengine ni mkewe Wahu, Mr. Lenny, Kidum, Jua Cali, Big Pin, Necessary Noise, Bensoul, Habib na Manga kati ya wengine wengi.
Redsan naye anapanga kuadhimisha miaka 30 katika muziki Jumamosi Agosti 29, 2026 katika uwanja wa Carnivore huku orodha ya watakaotumbuiza siku hiyo, ikikaribia kufanana na ya Nameless.
Kutoka nje ya nchi, Redsan amemwalika Jose Chameleone na Bebe Cool kutoka Tanzania na TID na AY kutoka Tanzania kati ya wengine.