Nameless athibitisha uwepo wa Wyre kwenye tamasha yake

Alimtaja Wyre kuwa rafiki anayemchukulia kama familia, akitafakari safari yao ya pamoja tangu walipoanza kujijenga katika muziki.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii nguli wa muziki nchini Kenya, Nameless, amemsifia msanii mwenzake Wyre huku shamrashamra zikiongezeka kuelekea tamasha yake inayosubiriwa kwa hamu ya ‘NamelessAt25’.

Kupitia ujumbe wa kugusa hisia, Nameless alimwelezea Wyre kama rafiki anayemchukulia kama familia, akitafakari safari yao ya pamoja tangu walipoanza kujijengea majina katika tasnia ya muziki.

Nameless alikumbuka alivyokutana na Wyre baada ya kushinda shindano la kurekodi muziki na mtayarishaji Tedd Josiah katika studio za Audio Vault, ambapo Wyre alikuwa akifanya kazi kama mtayarishaji msaidizi.

Urafiki wao ulikua kupitia muziki, huku Nameless akisema kuwa wimbo maarufu wa Wyre, Chuki, ulimvutia sana wakati wa enzi za Ogopa Deejays.

Kwa miaka mingi, wasanii hao wawili wamekuwa wakishiriki jukwaa moja, kuimba katika harusi za kila mmoja, na kupeana msaada wakati wa mafanikio na changamoto katika maisha pamoja na tasnia ya burudani.

Kwa mujibu wa Nameless, uwepo wa Wyre katika sherehe za NamelessAt25 unawakilisha zaidi ya muziki, bali ni heshima kwa undugu wao wa kudumu na safari waliyoipitia pamoja.

Pia aliwahimiza mashabiki kupendekeza nyimbo za Wyre ambazo wangependa azitumbuize katika tamasha hilo la kihistoria.

Tamasha hiyo ya kuadhimisha miaka 25 ya Nameless katika tasnia ya muziki itaandaliwa Agosti 15 na 16, 2026 katika uwanja wa Carnivore jijini Nairobi.

Share This Article