Marekani iliendeleza mashambulizi dhidi ya Iran kwa usiku wa sita mfululizo, kulingana na jeshi lake, huku pande hizo mbili zikiendelea kupigania udhibiti wa Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Usimamizi wa upande wa Marekani katika vita hivyo, CENTCOM ilisema mashambulizi hayo yalilenga kuendelea kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran.
Ulisema pia kwamba ulikamata chombo cha majini kama sehemu ya operesheni yake ya kuzuia usafiri katika mlango huo wa bahari.
Katika kile kinachoonekana kuwa ongezeko la mvutano, vyombo vya habari vya serikali ya Iran viliripoti kuwa Marekani ilishambulia miundombinu ya kiraia, kama madaraja, kituo cha treni na uwanja wa ndege.
Makombora ya Marekani pia yalishambulia maeneo karibu na kisiwa cha Qeshm, kilicho karibu na mlango huo wa bahari, pamoja na Bandar Abbas na Bushehr, ambako kuna kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia.
CENTCOM haikutaja madaraja katika orodha yake ya malengo kadhaa ya kijeshi ya Iran iliyosema yalilengwa katika awamu ya hivi karibuni ya mashambulizi, yaliyomalizika alfajiri ya Ijumaa.
Ilisema ndege za kivita, droni na meli zilishambulia “maeneo ya ufuatiliaji wa pwani na ulinzi wa anga, miundombinu ya usafirishaji na ugavi wa kijeshi, pamoja na uwezo wa kijeshi wa baharini.”
Mapema wiki hii, Rais wa Marekani Donald Trump alitishia kushambulia madaraja na vituo vya kuzalisha umeme vya Iran iwapo nchi hiyo haingerejelea mazungumzo.
Baada ya Trump kusema mwezi Aprili kwamba Marekani ingeshambulia kwa mabomu miundombinu ya kiraia nchini Iran, kama madaraja na vituo vya umeme, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, alisema kuwa kushambulia kwa makusudi raia na miundombinu ya kiraia ni uhalifu wa kivita.