Wanajeshi wa EACRF washambuliwa

Marion Bosire
1 Min Read

Usimamizi wa kikosi cha pamoja cha mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambacho kinahudumu mashariki ya taifa la DR Congo, EACRF, umetoa taarifa kuhusu shambulizi dhidi ya wanajeshi wake.

Kwenye taarifa hiyo usimamizi huo unaelezea kwamba wanajeshi wake wa asili ya Uganda walishambuliwa Jumatatu Oktoba 16, 2023, walipokuwa njiani kutoka Kiwanja kuelekea Bunagana.

Inasemekana kwamba wanachama waliokuwa wamejihami wa kundi lisilojulikana walishambulia wanajeshi hao katika eneo la Rukoro, Burai kwenye barabara kuu ya kutoka Rutshuru kuelekea Bunagana lakini wanajeshi hao waliweza kukabili watu hao na kuendelea na safari yao na kuwasili salama.

Kulingana na taarifa hiyo, uchunguzi umeanzishwa ili kubaini utambulisho wa kundi hilo na lengo la shambulizi lao dhidi ya wanajeshi.

Kikosi cha EACRF kimetoa hakikisho kwamba kimejitolea kuendelea kulinda raia huku kikihakikisha uzingatiaji wa sera za kikazi na sera zinazoongoza kazi yao katika eneo la mashariki la nchi ya DR Congo.

Website |  + posts
Share This Article