Waziri wa ulinzi nchini Kenya Aden Duale amesema kwamba wanajeshi wa KDF watatumwa katika kaunti zote 47 kusaidia maafisa wa polisi kudumisha amani na usalama.
Hatua hii inajiri kufuatia maandamano yaliyoshuhudiwa humu nchini ambayo yalisababisha vifo vya takribani watu 23.
Kupitia arifa ya gazeti rasmi la serikali, waziri Duale alisema kwamba Duale alielezea kwamba jukumu kuu la KDF litakuwa kulinda miundomsingi muhimu na kulinda maisha na mali ya wakenya.
Wakati wa maandamano siku ya Jumanne, waandamanaji waliingia katika bunge la taifa sehemu ambayo huwa chini ya ulinzi mkali baada ya kuwazidi nguvu polisi waliokuwepo.
Waandamanaji hao wanadaiwa pia kuchoma afisi za kaunti ya Nairobi huko City Hall, jijini Nairobi. Visa vya uporaji na uharibifu wa mali vilishuhudiwa pia katika sehemu mbali mbali nchini.
Waziri Duale alielezea kwamba wanajeshi hao watasalia nyanjani hadi pale ambapo utulivu utarejea nchini kikamilifu.
Awali hatua ya kutuma wanajeshi hao nyanjani iliyoratibishwa bungeni ilikumbwa na kikwazo cha keshi ya kuipinga mahakamani lakini mahakama kuu ikaikubalia.
Mahakama hiyo ilitambua umuhimu wa wanajeshi kusaidia polisi lakini jaji Lawrence Mugambi akaitaka serikali kuainisha namna wanajeshi hao watatumwa nyanjani na watakuwepo kwa muda gani.