Wanahabari kuandamana wiki ijayo kulalamikia ukatili wa polisi

Marion Bosire
2 Min Read

Chama cha wanahabari nchini Kenya Union of Journalists – KUJ kimetangaza kwamba wanahabari wataandaa maandamano kote nchini Jumatano wiki ijayo kulalamikia ukatili wa maafisa wa polisi.

Haya yanafuatia kisa cha mwanahabari wa kampuni ya Mediamax kwa jina Catherene Kariuki kupigwa risasi na maafisa hao wa usalama huko Nakuru jana wakati wa maandamano.

Katibu mkuu wa KUJ Eric Oduor jana kupitia taarifa alilaani kisa hicho akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya maafisa wa polisi aliowataja kuwa watepetevu kazini.

Aliitaka mamlaka ya kutathmini utendakazi wa polisi IPOA kutekeleza uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya maafisa watakaopatikana na hatia.

Bi. Catherine Kariuki amelazwa katika hospitali moja huko Nakuru baada ya kujeruhiwa mguu na risasi iliyofyatuliwa na afisa wa polisi.

Awali rais wa chama cha wahariri nchini Kenya Editors Guild Zubeda Koome alihutubia wanahabari katika kituo cha polisi cha Karen walikofika kuhakikisha usalama wa mwanahabari mkongwe Macharia Gaitho.

Kananu ambaye alikuwa amejawa na hamaki alitishia kutoa ilani ya siku saba ya mgomo na maandamano ya wanahabari kufuatia ukatili wa maafisa wa polisi.

Gaitho anasemekana kukamatwa na kudhulumiwa na maafisa wa usalama katika kile walichokitaja kuwa kisa cha kumdhania kuwa mtu mwingine ambaye anachunguzwa na polisi.

Hatua hii imeafikiwa wakati ambapo wanahabari mjini Kiambu wameandamana kulalamikia ukatili huo wa polisi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *