Takriban watu 53 wanaripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa usiojulikana ndani ya siku moja tangu kugundulika kwa dalili za ugonjwa kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC).
Shirika la Afya duniani (WHO) linasema hatari ya ugonjwa huo kuenea kimataifa ni ndogo na linachunguza kwa kina kuhusu ugonjwa huo wa ajabu, na chanzo chake.
Vifo hivyo vinajulikana kutokea kwa muda wa wiki mbili mwezi Februari, katika kijiji kimoja huko Basankusu, jimbo la Equateur.
Hakuna uhusiano na virusi vya Ebola na Marburg.kwa mujibu wa matokeo ya vipimo vya maabara.
Nusu ya wagonjwa walikuwa na malaria.
Wataalam sasa wanachunguza ikiwa ni viashiria vya homa ya uti wa mgongo miongoni mwa watu ambao tayari walikuwa na maambukizi mengine kama vile malaria.
Pia wamekusanya maji na sampuli nyingine za mazingira ili kuchunguza zaidi.
Kifo cha mwisho kiliripotiwa tarehe 22 mwezi uliopita na hakuna ushahidi wa maambukizi zaidi katika kijiji hicho kilichoathiriwa.
Awali vifo vilitokea miongoni mwa makundi yote ya umri lakini viliathiri zaidi wavulana na wanaume vijana.
Zaidi ya watu elfu moja mia tatu wenye dalili za ugonjwa huo walitambuliwa.