Wanahabari Kiambu waandamana, walaani kupigwa risasi kwa Catherine Wanjeri

Martin Mwanje
2 Min Read

Wanahabari mjini Kiambu wameandamana leo Jumatano kulalamikia kupigwa risasi kwa mwenzao mjini Nakuru wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z jana Jumanne. 

Wamelaani vikali kupigwa risasi kwa mwanahabari wa kampuni ya Mediamax Catherine Wanjeri ambaye alikimbizwa hospitalini ili kuondolewa risasi pajani.

Wanahabari hao walioandamana hadi makao makuu ya polisi ya kaunti ya Kiambu leo asubuhi wamewataka maafisa wa polisi kuwaacha kufanya kazi yao bila kutishiwa.

Ripoti zinaashiria kuwa shughuli ya upasuaji ya kumuondoa Wanjeri risasi pajani imefanikiwa.

Kulingana na mwanahabari Mumbi Wambugu ambaye alizungumza na KBC kwa njia ya simu jana Jumanne, Wanjeri awali alikuwa amepelekwa kwenye hospitali ya Valley lakini baadaye akahamishwa hadi hospitali kuu ya Nakuru.

Mwanahabari huyo alipigwa risasi ya mpira mara tatu kwenye paja lake licha ya kuwa alikuwa amevalia sare rasmi ya wanahabari na kuvalia kitambulisho chake cha uanahabari. Hali yake kwa sasa inasemekana kuimarika.

Mwanahabri wa Mediamax Catherine Wanjeri apigwa risasi akiwa kazini wakati wa maandamano kaunti ya Nakuru.

Kisa hicho kilishtumiwa vikali na wadau wa sekta ya vyombo vya habari ambao walitaka hatua kuchukuliwa dhidi ya afisa wa polisi aliyehusika kwenye kisa hicho.

Rais wa Chama cha Wahariri wa Habari, KEG Zubeida Kananu na Katibu Mkuu wa Chama cha Wanahabari Eric Oduor katika taarifa walitoa wito wa kulindwa kwa wanahabari wakiwa kazini.

Kwa upande wake, Baraza la Wanahabari nchini, MCK limewahimiza wanahabari kuzingatia usalama wao wanapokuwa kazini.

“Tunatoa wito kwa wanahabari kuhakikisha usalama wao na kutekeleza utaalam wanapofanya kazi katika mazingira hatari,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa MCk David Omwoyo.

Website |  + posts
Share This Article