Katibu katika Wizara ya Elimu Dkt. Belio Kipsang amewaagiza wanafunzi wote hapa nchini kujisajili kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii, SHIF kabla ya shule kufunguliwa wiki ijayo kwa muhula wa tatu.
Kupitia kwa barua iliyoandikwa tarehe 16 mwezi huu kwa wakuu wa elimu wa maeneo na kaunti, Dkt. Kipsang alisema Wakenya wote wanahitajika kikatiba kujisajili kwa hazina hiyo, na kuwaagiza wanafunzi wote wajisajili kama wategemeaji wa wazazi wao.
Wanafunzi wanaweza kujisajili kwa hazina hiyo kupitia tovuti yake rasmi ya afyaangu.go.ke au kwa kutumia USSD Code *147#.
Kipsang alisema iwapo watakumbwa na changamoto zozote za usajili, wanashauriwa kuwasiliana na halmashauri ya afya kwa jamii kupitia nambari ya simu 0800720601 au info@sha.go.ke.
Shughuli ya kujisajili kwa hazina hiyo ilianza tarehe mosi mwezi Julai mwaka huu.