Wanafunzi wa utabibu wa chuo cha KU kunoa makali yao katika hospitali ya KUTRRH

Tom Mathinji
1 Min Read
Hospitali maalum ya mafunzo na utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH) .

Awamu ya kwanza ya wanafunzi mia moja wa chuo kikuu cha Kenyatta wanaosomea taaluma ya matibabu, watapata fursa ya kutumia vifaa vya hospitali maalum ya rufaa, mafunzo na utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH) mapema wiki ijayo, kufuatia idhinisho la baraza la madaktari na wataalamu wa meno nchini (KMPDC).

Kulingana na afisa mkuu mtendaji wa hospitali hiyo ya kiwango cha level 6 Ahmed Dagane, iko tayari kuwapokea wanafunzi hao kulingana na kanuni zilizotolewa na baraza la chama cha madaktari na wataalam  wa meno.

Kama sehemu ya mapokezi kwa wanafunzi hao, Dagane amesema hospitali hiyo imeandaa mafunzo ya siku mbili ya kuwafahamisha wanafunzi pamoja na wasimamizi wao mambo ya kimsingi ambayo yameratibiwa Jumatatu wiki ijayo.

“Mafunzo ya utabibu hapa nchini yanatekelezwa chini ya kanuni dhabiti kuhakikisha ubora wa hali ya juu. Sheria za kutumia vifaa hivi zimewekwa bayana na kutumwa pia kwa chuo kikuu cha Kenyatta, kufanikisha hatua ya kujiunga kwa wanafunzi 100 wa utabibu,”alisema Dagane.

Watakapo wasili katika hospitali hiyo, wanafunzi hao watapelekwa katika wodi tano, kitengo cha wagonjwa wa figo na idara ya enkolojia, kama vile kitengo cha matibabu bila upasuaji, kitengo cha matibabu ya saratani miongoni mwa vitengo vingine.

Share This Article