Wanafunzi hasa wa shule za upili wamehimizwa kukumbatia somo la Kifaransa kama njia mojawapo ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa ajira miongoni mwa vijana hapa nchini.
Ni wito ambao umetolewa na wadau wa lugha ya Kifaransa katika hafla ya mashindano ya kutahini wanafunzi wa somo hilo kutoka shule mbalimbali za upili ambayo iliandaliwa katika shule ya upili ya wavulana ya Machakos.
Akizungumza katika hafla hiyo mhadhiri wa somo la Kifaransa katika chuo kikuu cha TUM Dkt. Teresa Otieno alisema kuna nafasi nyingi za ajira ambazo zimebuniwa na ubalozi wa Ufaransa humu nchini kwa vijana wanaoelewa lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wao, walimu wa lugha hii katika shule zaidi ya 50 za upili zilizohudhuria mashindano hayo wakiongozwa na Cynthia Kerubo wa shule ya upili ya wasichana ya Makueni walisema kwa sasa, kunashuhudiwa ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na somo la Kifaransa katika shule hizo.
Fridah Mueni mwanafunzi wa shule ya wasichana ya Makueni aliyeshiriki mashindano hayo alisema alichagua somo hilo kama mbinu mbadala ya kumweka katika nafasi bora ya kupata ajira siku za usoni
Shirika lisilo la kiserikali lililoandaa mashindano haya kwa jina Kifaransa village kupitia kwa rais wake Monsieur Sammy Simiyu linasema limechukua hatua hii ili kusaidia wanafunzi wa sasa kuboresha ujuzi wao wa lugha hii ili kuimarisha nafasi yao ya kupata kazi kabambe ambazo zinajitokeza kwa watalaam wa lugha hii.