Chama cha Madaktari, Wataalamu wa Dawa na Meno nchini (KMPDU), kimesema wanachama wake wanaogoma hawatatiwa hofu na vitisho.
Akiwahutubia wanahabari baada ya kuandaa mkutano na madakatari katika kaunti ya Kirinyaga, Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Atellah alisema hatua ya waajiri kutoa vitisho kwa madakatari wanaogoma ni jambo la kusikitisha.
Atellah alisema maswala yaliyoibuliwa na wahudumu hao wa afya hayafai kuingizwa siasa ila yanafaa kupewa umuhimu ili kuimarisha maslahi yao na ile ya sekta ya afya.
Amewataka Magavana, wasimamizi wa hospitali za rufaa na Wizara ya Afya kuwalipa madaktari marupurupu yao ya miaka saba.
Alitaka hatua ya kuwapandisha vyeo madaktari kuharakishwa, akidokeza kuwa madaktari wengi wamekuwa katika kiwango kimoja cha kazi kwa zaidi ya miaka 15.
Madaktari wamegoma tangu Machi 14 kulalamikia ukosefu wa serikali wa kuwaajiri madaktari wanagenzi na kushindwa kwa Wizara ya Afya kutekeleza mkataba wa nyongeza ya mishahara ya madaktari wa mwaka 2017.
Mashauriano baina ya KMPDU na Wizara ya Afya hayajafanikiwa huku madaktari hao wakiishtumu serikali kwa kutotii maagizo ya mahakama.