Wanafunzi zaidi ya 9,000 kutoka eneo bunge la Narok Mashariki, watanufaika na ufadhili wa karo wa shilingi milioni 30 kutoka kwa hazina ya serikali ya kitaifa ya maendeleo ya maeneo bunge (NG-CDF) mwaka wa fedha 2022/2023.
Mbunge wa Narok Mashariki Ken Aramat amesema watakaonufaika walituma maombi kwa njia ya kidijitali huku maombi yao yakiidhinishwa na machifu wao.
Kulingana na mbunge huyo, mfumo huo wa kidijitali huhakikiaha uwazi na uwajibikaji, huku wanaotuma maombi bila kuzingatia miegemeo yao ya kisiasa wakinufaika na hazina hiyo.
Aidha, alidokeza kuwa idadi ya wanaotuma maombi imeongezeka kutoka 3,000 mwaka 2013 hadi 9000 katika mwaka wa sasa wa kifedha huku akiwapongeza wakazi kwa kuwapa watoto wao elimu.
Hata hivyo, mbunge huyo alisema changamoto kuu inayokumba utumaji maombi kwa njia ya dijitali ni kwamba wanafunzi kutoka maeneo bunge jirani pia hutuma maombi katika eneo bunge hilo.
Wakazi walisifu mchakato huo wakisema watu wote walinufaika na mchakato huo.