Serikali ya kaunti ya Kakamega imetia saini hati ya maelewano na shirika la kimataifa la Global Civic Sharing Organization (GCS) kwa faida ya wafanyabiashara wa bodaboda.
Kwa mujibu wa hati hiyo, shirika hilo la taifa la Korea Kusini litafadhili mafunzo ya Bodaboda kwa shilingi milioni 30 likishirikiana na mamlaka ya usasfiri na usalama wa barabarani(NTSA).
Makubaliano hayo ya miaka miwili pia yatatoa ruzuku ya kupiga jeki biashara hiyo.
Baada ya maelewano hayo, mwanachama wa kamati ya utendaji ya huduma za jamii, michezo, vijana, jinsia na utamaduni Moffart Mandela, alisema kuwa mpango huo utasaidia kuboresha maisha ya wanabodaboda kwa kuwapa ujuzi wa barabarani.
Aliongeza kuwa GCS ina uhusiano wa muda mrefu na kaunti hiyo kwani imekuwa ikiwafadhili wafanyakazi vijana, wanawake na wafanyakazi wa kaunti hiyo.
”Kupitia shirika hili, na lile la ushirika wa kimataifa wa Korea (KOICA), tumepata fursa nyingi za wafanyakazi wetu kusafiri nchini Korea ambazo ziliungwa mkono na serikali ya Korea na kufadhiliwa na GCS kwa lengo la mafunzo ya kuinua vijana na wanwake,” alisema Mandela.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa mkuu wa GCS Hyunju Cho alisema kuwa mpango huo unalenga waendeshaji wa bodaboda 240 kutoka kunti ya Kakamega na idadi hiyo itaongezeka siku za usoni.
Pia alifichua kuwa shirika hilo lina mpango sawia katika kaunti ya Uasin Gishu ambao umefanikiwa.