Wakuliwa wameshauriwa kununua mbolea kutoka kwa mawakala walioidhinishwa na serikali, kuepuka kuhadaiwa kwa kuuziwa mbolea ghushi zitakazoathiri mazao yao.
Meneja wa eneo la mlima Kenya wa shirika la ufadhili wa kilimo AFC, Erick Mutai, alisema baadhi ya mawakala hununua mbola kutoka kwa serikali na kisha kuichanganya na mbolea bandia kabla ya kuwauzia wakulima.
Kulingana na meneja huyo, serikali inajizatiti kuwauzia wakulima mbolea ya gharama nafuu, ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kuhakikishia taifa hili usalama wa chakula.
Akizungumza katika halmashauri ya nafaka na mazao mjini Isiolo, Mtai alisema serikali kupitia shirika la ufadhili wa kilimo,AFC, imewawezesha wakulima kupata mikopo kwa riba ya asilimia 10.
Kwa upande wake meneja wa NCPB tawi la Isiolo Rosekellen Njiru, alisema shehena ya kwanza ya magunia 1,800 ya mbolea kutoka kwa serikali imewasili, na sasa inasubiri kununuliwa na wakulima, huku akiwahimiza kujihadhari kuhadaiwa na mawakala.
Alisema wakulma wote ambao wamesajiliwa katika eneo hilo na serikali, watanufaika na mbolea hiyo ya bei nafuu.