KRA yazindua vituo vya uwezeshaji biashara Turkana

Martin Mwanje
1 Min Read
Kamishna Mkuu wa KRA Humphrey Wattanga akiongoza uzinduzi wa vituo vya uwezeshaji biashara

Mamlaka ya Mapato nchini (KRA) imezindua vituo vya uwezeshaji biashara katika eneo la Kainuk, Lodwar na Kakuma, kaunti ya Turkana katika hatua inayotarajiwa kupiga jeki biashara kati ya Kenya na Sudan Kusini. 

Uzinduzi wa vituo hivyo uliongozwa na Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo Humphrey Wattanga.

Vituo hivyo vinalenga kuboresha biashara katika kile kinachojulikana kama Ushoroba wa Kaskazini, ambayo ni njia muhimu ya biashara inayounganisha mataifa ya Kenya na Sudan Kusini, Ethiopia na Uganda.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Wattanga alisifia uzinduzi huo akisema utasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha biashara katika eneo la Afrika Mashariki.

“Vituo hivyo ni muhimu katika usafirishaji wa biadhaa ndani ya eneo hili na vinatarajiwa kuboresha utendakazi wa KRA kwenye barabara unganishi ya Sudan Kusini,” alisema Wattanga.

“Hii leo, tunasherehekea mafanikio makubwa katika uwezeshaji wa biashara na usalama wa mpakani. Mradi huu utahakikisha mipaka yetu ni salama, mazingira yetu ya biashara yanasalia kuwa mazuri, na jamii kwa jumla inalindwa,” aliongeza Wattanga.

 

Website |  + posts
Share This Article