Wakenya zaidi ya 600,000 wasajiliwa chini ya mpango wa Inua Jamii

Martin Mwanje
1 Min Read

Wakenya 601, 539 wanaostahiki kusajiliwa chini ya mpango wa Inua Jamii walisajiliwa na serikali kufikia leo Jumatatu asubuhi. 

Mpango huo unalenga kuwasajili wazee, watoto mayatima, watoto wasiojiweza na watu wanaoishi na ulemavu.

Serikali inalenga kuongeza idadi ya watu wanaonufaika chini ya mpango wa Inua Jamii kutoka idadi ya sasa ya watu milioni 1.2 hadi milioni 2.5.

“Tafadhali, ibainike kuwa mipango ya kuhamishia pesa taslimu kwa mayatima (CTOVC), watoto wasiojiweza na watu wenye ulemavu, PWSD itafanyiwa ukaguzi zaidi ili kubaini wale wanaostahiki kunufaika,” amesema Waziri wa Leba Florence Bore.

Bore, aliyezungumza wakati akiangazia zoezi la usajili wa watakaonufaika na mpango huo mjini Nyeri leo Jumatatu, amesema shughuli ya usajili inaendelea vyema na itaendelea hadi mwishoni mwa mwezi huuu.

Waziri ametoa hakikisho kuwa hakuna Mkenya atakayefungiwa nje ya zoezi hilo akisisitiza dhamira ya serikali kutoa usaidizi kwa wale wasiojiweza zaidi katika jamii.

“Kwa mujibu wa Ajenda ya Kenya Kwanza ya kutoka Chini kwenda Juu ya kuibadilisha nchi, Wizara yangu inaongeza idadi ya watakaonufaika na mpango wa Inua Jamii kwa watu 500,000 kama ilivyoelekezwa na Rais Ruto,” alisema Bore.

Waziri amewaelekeza maafisa husika kuhakikisha mchakato wa usajili unaharakishwa na kuendeshwa ipasavyo.

Share This Article