Wakenya wanaoishi Msumbiji wahimizwa kudumisha utamaduni

Tom Mathinji
2 Min Read

Rais Ruto amewahakikishia Wakenya walioko ughaibuni kwamba Serikali itaendelea kufanya mageuzi yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma.

Alisema jitihada zinafanyika kuhakikisha huduma zote za Serikali zinahamishiwa katika mfumo wa kidijitali ili kuwawezesha kupata huduma mtandaoni bila ya kulazimika kutembelea ofisi husika.

“Niliposhika madaraka mwaka jana, huduma 320 za Serikali zilikuwa zikifanywa mtandaoni. Lakini sasa tuna huduma 5,300 mtandaoni. Nina hakika kufikia mwisho wa mwaka huu, huduma zote zitakuwa zinafanyika mtandaoni,” alisema.

Akiwahutubia Wakenya wanaoishi Msumbiji mjini Maputo, siku ya Ijumaa jioni, Dkt Ruto alisema suala la leseni za udereva ambalo limekuwa changamoto kwao nchini Msumbiji limetatuliwa.

“Tumehitimisha na kutia saini utambuzi wa leseni za udereva za nchi zetu mbili. Sasa mnaweza kutumia leseni zenu za udereva kutoka Kenya nchini Msumbiji bila tatizo lolote,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto zaidi aliwataka kuendeleza utamaduni wa kuweka akiba.

“Ni wakati wa kuanza kuweka akiba na kuwekeza katika miradi ambayo itatusaidia katika siku zijazo.

“Utamaduni wa kuweka akiba ndiyo njia pekee ya kufanikiwa,” alisema Dkt Ruto.

Alisema Serikali imeifanyia mabadiliko Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) ili kuhakikisha utoaji wa huduma kwa ufanisi.

Viongozi waliohudhuria ni Mawaziri Alfred Mutua (Masuala ya Kigeni), Aden Duale (Ulinzi) na Mwanasheria Mkuu Justin Muturi miongoni mwa wengine.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *