Wakenya wamehimizwa kuripoti mara moja visa vya mizozo kati ya binadamu na wanyamapori kwa shirika la huduma kwa wanyamapori KWS kupitia nambari 0800597000.
Maelekezo haya yanajiri baada ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Multi Media huko Rongai kufanya maandamano kulalamikia kushambuliwa kwa mwenzao na fisi.
Wanaoishi karibu na eneo hilo wanahimizwa kuwa waangalifu wasije wakashambuliwa na wanyamapori kwani eneo la kusini la mbuga ya Nairobi halina ua na ndilo mapito ya wanyama wanaohama.
Kupitia taarifa, KWS imeelezea kwamba watu wawili mmoja wao akiwa mwanafunzi wa MMU walishambuliwa na fisi kwenye barabara ya Ole Kasasi huko Rongai kaunti ya Kajiado jana saa mbili usiku.
Maafisa wa KWS walifika kwenye eneo hilo punde baada ya kufahamishwa na kuokoa wawili hao ambao walipelekwa kwenye hospitali ya Wema kwa huduma ya kwanza na baadaye kupelekwa kwenye hospitali kuu ya Kenyatta.
Mabaki ya mtu mwingine mmoja yalipatikana katika eneo hilo na kulingana na KWS yametambuliwa na familia yake kufahamishwa.
Fisi mmoja aliuawa na maafisa wa KWS na wanachunguza mabaki yake kubaini iwapo alikuwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa na magongwa mengine.
Maafisa hao bado wamekita kambi katika eneo hilo kutafuta maficho ya fisi na kuwarejesha kwenye mbuga ya Nairobi.